MO Dewj Billionea wa 13 Afrika

Katika orodha hiyo ya jarida mashuhuri la Forbes linalofuatilia utajiri wa watu kwa mwaka huu limemtaja Mo mwenye miaka 45 kama bilionea namba 13 akitoka nafasi ya 17 mwaka jana huku mfanyabiashara wa saruji, sukari na unga (Aliko Dangote wa Nigeria) akiendelea kuongoza orodha hiyo.


Mo pic

Inaelezwa kuwa utajiri wa Mo wa sasa ni Dola za Marekani bilioni 1.6 (Sh3.7 trilioni) na anayeshikilia namba moja utajiri wake ni Dola 12.1 bilioni (Sh28.9 trilioni).

Katika orodha ya jarida hilo ya Januari mwaka jana, Mo anayefanya biashara mchanganyiko alikuwa nafasi ya 17 akiwa na utajiri huohuo wakati mwaka juzi alishika nafasi ya 14 akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.9.

Mwaka jana baada ya utajiri wake kupungua kwa Dola milioni 300 (Sh695.7 bilioni) na kushuka nafasi tatu katika orodha ya matajiri Afrika alilieleza gazeti hili kuwa mwaka ulioisha ungekuwa wa neema. “Imepungua Dola milioni 300 (Sh692.67 bilioni ya wakati huo), lakini nina watu 32,000 na mwaka huu natarajia kuwekeza Sh500 bilioni hapahapa nchi na uwekezaji huo utatoa ajira 100,000 kwa Watanzania,” alisema Mo baada ya ripoti hiyo.

Jana, Mo Dewji alipotafutwa kuzungumzia kuwemo kwenye orodha hiyo, alisema anashukuru mchango wake umeendelea kutambulika ndani ya nchi na nje ya nchi.

Alisema dhamira yake ni kuhakikisha anaendelea kusaidiana na Serikali katika kujenga uchumi wa Tanzania na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

“Niko bega kwa bega na Serikali ya Dk John Magufuli na nafarijika sana kutokana na mageuzi makubwa anayoendelea kuyafanya kwenye sekta ya viwanda.

Fursa za uanzishaji viwanda kwa sasa ni nyingi na namuomba Mungu aniwezeshe kufikia malengo yangu ya kuanzisha viwanda vipya kati ya vitano hadi 10 katika mwaka huu mpya,” alisema Mo Dewji ambaye ni mwekezaji wa Klabu ya Simba.

Pia alisema kuwa ahadi aliyoitoa kwenye kundi la matajiri duniani kwamba, asilimia 50 ya utajiri wake itaelekezwa kwenye kusaidia makundi yasiyojiweza iko palepale.

“Unapobarikiwa na Mungu ni muhimu kuwatazama wengine pia, hivyo ile ahadi yangu ya kurejesha asilimia 50 ya utajiri kwa makundi yenye mahitaji na yasiyojioweza iko palepale,” alisema.

Jarida hilo limemtaja Aliko Dangote (63) mfanyabiashara wa saruji na sukari wa Nigeria kuongoza orodha hiyo akiwa na utajiri wa dola 12.1 bilioni.

Wa pili ni Nassef Sawiris wa Misri (60) akiwa na utajiri wa dola 8.5 bilioni. Biashara zake ni ujenzi na uwekezaji. Nafasi ya tatu imeshikwa na Nicky Oppenheimer (75) ambaye ni mfanyabiashara wa almasi wa Afrika Kusini na nafasi ya nne imeshikwa na Johann Rupert (70) anayefanya biashara ya vitu vya anasa huku wa tano akiwa Mike Adenuga (67), mfanyabiashara wa kampuni za simu na mafuta nchini Nigeria mwenye utajiri wa dola 6.3 bilioni.

Mwingine ni Abdulsamad Rabiu pia kutoka Nigeria akimiliki utajiri wa dola 5.5 bilioni kutokana na viwanda vya saruji na sukani.

Wengine ni pamoja na Issa Rebrab (77) kutoka Algeria akifanya biashara za vyakula na utajiri wake unafikia dola 4.8 bilioni. Yupo pia Naguib Sawiris kutoka Misri (66) akiwa na utajiri wa dola3.2 bilioni kutokana na biashara ya kampuni za simu na pia yupo Patrice Motsepe kutoka Afrika Kusini mwenye utajiri wa dola3 bilioni akifanya biashara za madini.

Wengine ni pamoja na Koos Bekker (68) kutoka Afrika Kusini akifanya biashara za vyombo vya habari, yupo pia Mohamed Mansour kutoka nchini Misri akishika nafasi ya 11 katika orosha hiyo.

Nafasi ya 12 imeshikwa na Aziz Akhannouch kutoka Morocco mwenye utajiri wa dola 2bilioni na nafasi ya 14 imeshikwa na Yoseph Mansour kutoka Misri.

Nafasi ya 15 imeshikwa na Othman Benjelloun, ya 16 imeshikwa na Michiel Le Roux, ya 17 imeshikwa na Strive Masiyiwa na 18 imeshikwa na yassseen Mansour mwenye utajiri wa dola 1.1 bilioni.

Na Emmanuel kasomi

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Historia Ya Remmy Ongala

Mfahamu Sarah Martin Simbaulanga

Historia ya Dr. Livingstone